Mkuu wa Wilaya ya Sengerema mhe. Senyi Ngaga amewaagiza watendaji wa kata na vijiji Wilayani Sengerema kuhakikisha wanashirikisha wazazi na viongozi kuhusu suala ya lishe kwa wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo leo (29.05.2024) wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa Mikataba ya Lishe kilichowakutanisha watendaji wa kata na wataalamu ngazi ya Halmashauri.
Mkuu wa Wilaya amesema pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kufanya vizuri kwenye utekelezaji wa shughuli za Lishe bado suala la chakula kwa wanafunzi limekuwa halitekelezwi ipasavyo hivyo amewataka watendaji kupitia vikao vya ngazi za vijiji na kata kuwahusisha wazazi, walezi pamoja na viongozi ili kwa umoja wao waweke mikakati ya utoaji wa chakula shuleni na kulifanya kuwa suala endelevu.
"Fanyeni vikao vya wazazi na madiwani, wahamasisheni kuhusu suala la lishe kwa wanafunzi kuwa ni suala la lazima, mtoto akipata hata kikombe cha uji itasaidia" amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amewagiza watendaji wa kata kuhakikisha wanatoa elimu ya uhifadhi wa chakula kwa wananchi kwani baadhi yao wameanza kuuza na kusababisha kaya nyingi kukubwa na janga la njaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema akimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika kikao hicho amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema inaendelea kutekeleza vyema suala la lishe na amesema hadi kufikia mwezi Juni 2024 Halmashauri itakuwa imefikia lengo la kitaifa kuhusu utekelezaji wa mipango ya Lishe.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Dkt. Fredrick Mugarula amesema Halmashauri imekuwa ikifanya vizuri katika utekelezaji wa afua za lishe kutokana na ushirikiano kutoka kwa watendaji wa kata na vijiji ambao wameweka mikakati mizuri hivyo amewaomba kuendeleza ushirikiano huo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.