Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Kigoma Malima amewaagiza wataalamu wa kilimo waliopo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wakulima wa zao la Pamba waliopo mkoani wa namna bora ya uzalishaji wa zao hilo hili kuongeza uzalishaji kutoka kilo 150 za sasa hadi kufikia kilo 500 hadi 600 kwa hekari moja.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa agizo hilo wakati akizindua msimu wa upandaji wa zao la Pamba uliofanyika kata ya Nyapande na kuhudhiriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wilaya pamoja na wakulima.
Amesema Maafisa ugani waliopo katika halmashauri zote wanatakiwa kuhakikisha wanawatambua wakulima wa mfano wa zao la Pamba waliopo katika maeneo yote ya Wilaya za Mkoa wa Mwanza ili waweze kuwapatia elimu bora ya kilimo cha zao la Pamba kuanzia hatua ya upandaji hadi kuvunwa kwake.
"Mimi ninataka kuanzia msimu huu, uzalishaji wa Pamba uwe wa wastani wa kilo 500 hadi 600 kwa hekari 1 na si kilo 150 kama ilivyo, ninyi maafisa ugani ndio wa kutoa elimu juu ya kilimo chenye tija kwa wakulima wote wa zao la Pamba hususani kwa wale wakulima wa mfano" alisema Mhe. Malima.
Sambamba na hilo Mhe. Malima ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza kuanzisha mashamba darasa ya Wilaya ili wakulima wote wa zao hilo wajifunze kwa vitendo.
Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe.Hamis Tabasamu amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 150 za ruzuku ya mbolea kwa wakulima kote nchini hivyo amewataka wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo.
Mhe.Tabasamu pia amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha serikali inawachukulia sheria kali wauzaji wa pembejeo feki ili kukomesha tatizo hilo ambalo kwa sasa limekuwa ni tatizo sugu.
Mapema akitoa taarifa ya uzinduzi wa zoezi hilo kwa Mkuu wa Mkoa Afisa ugani ndugu Isack Shija amesema kwa sasa wataalamu wa kilimo wanasisitiza upandaji wa zao la Pamba unaotumia vipimo vya sentimita 60 msitari hadi msitari hadi mwingine na sentimita 30 shina moja hadi jingine ambapo hekari moja huweza kutoa miche 44,444 ambapo hapo hapo awali vipimo vilivyotumika vilikuwa ni sentimita 90 msitari mmoja hadi mwingine sentimita 40 shina hadi shina ambavyo viliweza kutoa miche 22,222 hivyo upandaji huu wa kisasa umeongeza tija kwa wakulima.
Msimu wa 2021/2022 Mkoa wa Mwanza ulifanikiwa kuzalisha tani 15,000 za zao la Pamba ambapo miongoni mwa hizo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilifanikiwa kuzalisha tani 3,199 ya lengo la kuzalisha tani 5,150.
Kwa msimu wa 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema inatarajia kuzalisha tani 5897 za Pamba.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.